UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MELI YA UVUVI BAHARI KUU

Kampuni ya Ogawa Seiki ya nchini Japani inayojenga Meli ya Uvuvi wa Bahari Kuu kupitia Serikali ya Japani chini ya mradi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii (ESDP Japan) imefanya ukaguzi wa eneo la ujenzi wa mfumo wa ufuatiliaji wa meli (site verification) 28 Julai 2025, katika Makao Makuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) yaliyopo Ras Mkwavi, Feri- Kigamboni, ambapo utafungwa Mfumo wa Ufuatiliaji wa Chombo (VMS) utakaotumika katika shughuli za meli za TAFICO.
Meneja wa Ogawa Seiki Divisheni ya usafirishaji wa nje Bw. Koichi Kondo ameambatana na wataalamu wa kampuni mbia ya ndani (Local Partner) Electricool Tanzania Limited, kampuni ambayo ndiyo itakayofanya usimikaji wa minara miwili (Wide Band Dipole Antenna) na ufungaji wa mfumo huo.
Mfumo wa Ufuatiliaji wa Chombo (Vessel Monitoring System) ni mfumo wa mawasiliano unaotumika kufuatilia, kudhibiti na kuchunguza shughuli za uvuvi wa meli zinapokuwa baharini. Mfumo huu unatarajiwa kuanza kufungwa mwezi Septemba 2025 ili kuruhusu mawasiliano kati ya manahodha wa meli za TAFICO baharini na chumba cha udhibiti (control room) kitakachokuwa Makao Makuu.
Meli ya TAFICO kupitia mradi wa ESDP Japan imefikia 75% ya ujenzi na itakamilika na kuwasili nchini ifikapo mwezi Disemba 2025 tayari kwa shughuli za uvuvi wa bahari kuu.