Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

HISTORIA YA TAFICO

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ni Shirika la umma linalomilikiwa na Serikali ya Tanzania chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. TAFICO ina jukumu la kuendeleza tasnia ya uvuvi nchini kwa kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za bahari. Uendelezaji huu utafikiwa kwa kutelekeza miradi mikubwa ya uvuvi wa kibiashara ikiwa ni pamoja na Uvuvi wa Bahari Kuu (Exclusive Economic Zone) Shirika linalenga kukuza uzalishaji wa samaki nchini, kutoa fursa za ajira, kuimarisha usalama wa chakula, na kuchangia ukuaji wa jumla wa sekta ya uvuvi nchini na ukuaji wa uchumi.

Shirika pia linalenga kuimarisha ufugaji wa samaki ili kuongeza uwezo wa uzalishaji wa samaki nchini. Kwa kuwekeza katika teknolojia za kisasa za ufugaji wa samaki, uzalishaji wa  chakula cha samaki, na kutoa mafunzo kwa wafugaji wa samaki wa ndani, Shirika linafanya kazi  kwa dhamira ya kuimarisha sekta ya uvuvi ili iwe inayojitosheleza zaidi na rafiki kwa mazingira.

Vilevile, Shirika linafanya kazi ya kuboresha mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi kwa kuwekeza katika vifaa vya usindikaji wa samaki, na maghala ya ubaridi ili kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvuna, hasa  dagaa na samaki wadogo (pelagic fish). TAFICO pia inashirikiana na wavuvi wadogo kufanya biashara ili kuhakikisha uvuvi endelevu na uhifadhi wa rasilimali za baharini.

 Dhamira ya Serikali kuirejesha TAFICO inalenga kuimarisha shughuli zake za kibiashara zinazo ihakikishia uendelevu wa kifedha. Kwa kushirikisha sekta binafsi, hasa kupitia ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), TAFICO inaweza kuongeza mtaji na utaalamu wa ziada ili kuendeleza ukuaji na mafanikio ya shirika. Utaratibu huu  sio tu inakuza maendeleo ya kiuchumi lakini pia unakuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kwa manufaa ya pande zote.