SERIKALI YASHAURIWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI UENDESHAJI WA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO
SERIKALI YASHAURIWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI UENDESHAJI WA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO
Katika kufikia malengo ya uwekezaji mkubwa wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, Serikali imeshauriwa kushirikisha Sekta Binafisi katika uendeshaji wake (operational and maintanance) kwa kutumia mfumo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Ushauri huo umetolewa wakati wa kikao cha kwanza cha Kamati ya Ushauri ya Uendeshaji wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, kilichofanyika Februari 03, 2026 katika Makao Makuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) Ras Mkwavi, jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kuzindua kamati hiyo, wakati anamwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena, Mkurugenzi wa Uvuvi nchini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Mohammed Sheikh, ameeleza dhamira ya kamati katika kushauri na kuweka mwelekeo bora wa uendeshaji wa Bandari hiyo muhimu ya kimkakati kwa maendeleo endelevu ya uchumi wa nchi katika sekta ya uvuvi.
“Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko umefikia zaidi ya asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi 2026, ukiwa umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 280. Bandari hii ni mradi mkubwa wa kimkakati ambao utazalisha ajira zaidi ya 30,000 na unalenga kuimarisha Sekta ya Uvuvi na kukuza Uchumi wa Buluu,” aliongeza Prof. Sheikh.
Kwa upande wa miundombinu, Bandari hiyo ina matenki ya kuhifadhia mafuta yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 4 kwa ajili ya kuhudumia meli za uvuvi, jengo la kisasa la kuhifadhi samaki lenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,800, gati ambalo meli za uvuvi zipatazo 10 zinaweza kushusha kwa wakati mmoja, eneo la matengenezo ya meli na miundombinu wezeshi. Miundombinu hii inalenga kuongeza ufanisi wa shughuli za uvuvi na kupunguza upotevu wa mazao ya baharini.
Vilevile, kukamilika kwa ujenzi wa Bandari hiyo kutaenda sambamba na ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki karibu na Bandari, pamoja na uwekezaji katika meli za kisasa za uvuvi kwa Shirika la Uvuvi Tanzania na sekta binafsi, kama mkakati muhimu wa kuongeza thamani, ushindani na faida inayotokana na rasilimali za uvuvi, pamoja na kuongeza mapato kwa wavuvi na wawekezaji.
Katika kikao hicho, wajumbe wa kamati walisisitiza kuwa ili Serikali ifikie malengo ya uwekezaji mkubwa uliowekwa katika Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, ni muhimu kuzingatia uzoefu kutoka mataifa yaliyoendelea na yenye mifumo thabiti ya usimamizi wa rasilimali za bahari, kufuata hatua sahihi za kumpata mbia, hivyo kushauri kushirikisha Sekta Binafsi katika uendeshaji na matengenezo (operation and maintenance) ya Bandari hiyo kupitia mfumo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), hatua itakayoongeza ufanisi, teknolojia na ushindani katika uendeshaji wake. Kamati hiyo pia imeweka msingi muhimu wa ushauri na maandalizi ya uendeshaji wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, inayotarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu nchini.
Aidha, wajumbe wanaounda kamati hiyo wanatoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi zilizopo chini yake, Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), taasisi zinazoshughulikia usimamizi wa usafirishaji na miundombinu baharini, biashara pamoja na nishati.