Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

TAFICO YAANZA RASMI MRADI WA UKARABATI WA GHALA LA UBARIDI

Imewekwa: 05 February, 2026
TAFICO YAANZA RASMI MRADI WA UKARABATI WA GHALA LA UBARIDI

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) limeanza rasmi utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa ghala la ubaridi (Cold Storage) lililopo Makao Makuu ya Shirika Ras Mkwavi, jijini Dar es Salaam.

Mradi huo unaotekelezwa chini ya ufadhili wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) umeanza leo Februari 05, 2026, ukilenga kuboresha miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi na kuimarisha mnyororo wa thamani.

Utekelezaji wa mradi unafanywa na Kampuni ya Kabirirti Engineering Limited, na unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 90.

Akizungumza wakati wa kuanza kwa kazi za ukarabati, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Juvenalis Mushi, alisema kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika na mkandarasi yuko tayari kutekeleza mradi kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na muda uliopangwa.

“Mradi huu utatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora, usalama na ufanisi. Lengo letu ni kuhakikisha ghala la ubaridi linafanya kazi ipasavyo mara baada ya kukamilika, ili liweze kuhudumia mahitaji ya TAFICO na wadau wa sekta ya uvuvi,” alisema Mhandisi Mushi.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO Bi. Perpetua Massaga, akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TAFICO CPA Shaibu Matessa, amesema kuwa mradi wa ghala la ubaridi ni sehemu ya maandalizi muhimu ya Shirika kuelekea kuanza rasmi shughuli zake za uvuvi.

“Uwekezaji huu ni hatua muhimu katika kujenga msingi imara wa uendeshaji wa TAFICO. Ghala la ubaridi litaongeza uwezo wa kuhifadhi mazao ya uvuvi, kupunguza upotevu na kuongeza thamani ya mazao, sambamba na mkakati wa Serikali wa kukuza Uchumi wa Buluu,” alisema Bi. Massaga.

Mradi huu unatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha miundombinu ya uvuvi nchini, kuongeza fursa za kiuchumi, na kuwezesha TAFICO kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi mara baada ya kuanza shughuli zake za uzalishaji.