TAFICO YASAINI MKATABA UJENZI WA MELI TATU
Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) Agosti 24, 2026, limesaini makubaliano ya ujenzi wa meli tatu za uvuvi wa Bahari Kuu, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yamesainiwa kupitia Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo Dkt. Suleiman Kiula, ndc, na kushuhudiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, pamoja na wawakilishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema ujenzi wa meli hizo ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha Tanzania inatumia ipasavyo fursa zilizopo katika rasilimali za Bahari Kuu, huku akisisitiza umuhimu wa kuunganisha sayansi, teknolojia na uvuvi endelevu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani, amesema katika kipindi cha miezi tisa tangu Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akabidhiwe jukumu la kuiongoza Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Serikali imeendelea kuchukua hatua muhimu katika kulifufua na kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), ikiwemo hatua ya ujenzi wa meli hizo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, amesema Serikali ina mpango wa kuwa na jumla ya meli sita za uvuvi wa Bahari Kuu, ambapo meli nne zitakuwa Tanzania Bara chini ya usimamizi wa TAFICO na meli mbili zitakuwa Zanzibar.
Pia, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAFICO Prof. Yunus Mgaya, amesema upatikanaji wa vitendea kazi muhimu ikiwemo meli hizo tatu za uvuvi wa Bahari Kuu ni ishara ya mapinduzi makubwa yanayoendelea ndani ya Shirika na sekta ya uvuvi kwa ujumla.
Kwa TAFICO, utiaji saini wa makubaliano hayo unaweka hatua nyingine muhimu katika safari ya kulirejesha Shirika katika nafasi yake ya kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa kibiashara wa Bahari Kuu.