BODI YA TAFICO YARIDHISHWA KUKAMILIKA KWA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), imefanya ziara ya ukaguzi katika mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko, kwa lengo la kujionea hatua ya utekelezaji wa mradi, kukagua miundombinu na maandalizi yaliyofanyika kuelekea kuanza kwa matumizi ya bandari hiyo, na kutathmini fursa zitakazotokana na uwekezaji huo katika shughuli za uvuvi na uchumi wa buluu.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 20 Agosti 2026, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Yunus D. Mgaya, ambapo Bodi hiyo imepata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali ya bandari na kupata maelezo kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya kuanza kwa shughuli zake.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Prof. Mgaya, amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo, akieleza kuwa kukamilika na kuanza kufanya kazi kwa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya uvuvi nchini.
"Bandari hii ina nafasi kubwa katika kuongeza ufanisi wa shughuli za uvuvi, kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, pamoja na kutoa fursa za ajira na biashara. Nawahimize wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko kwa kuwekeza katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya uvuvi," aliongeza Prof. Mgaya.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, Dkt. Suleiman Kiula, ndc, amesema Shirika hilo linaendelea na mchakato wa kushirikisha sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha bandari hiyo inaendeshwa kwa ufanisi, kwa kutoa huduma wezeshi kwa viwango bora na nafuu ili kuvutia Meli nyingi kutumia bandari hiyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Dkt. Kiula amesema TAFICO inaendelea kutekeleza mikakati ya kushiriki kikamilifu katika kuendeleza shughuli za uvuvi wa kisasa na ukuzaji viumbe maji, ikiwemo uwekezaji katika Meli za uvuvi wa bahari kuu, uanzishaji wa mashamba ya kufuga samaki, miundombinu wezeshi, pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko ni mradi wa kimkakati unaolenga kuimarisha shughuli za uvuvi nchini. Miundombinu ya bandari hiyo inajumuisha gati lenye urefu wa mita 315 la kuhudumia meli za uvuvi.