TAFICO, JESHI LA WANAMAJI KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA UVUVI WA BAHARI KUU
Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Jeshi la Wanamaji la Tanzania (Tanzania Navy Command) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu na uzoefu katika kuimarisha shughuli za uvuvi katika Bahari Kuu na kuweka mkakati wa pamoja wa kusimamia rasilimali za bahari kwa maslahi mapana ya Taifa.
Majadiliano hayo yamefanyika wakati Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, Dkt. Suleiman Kiula, ndc (T), alipofanya ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Kigamboni, Dar es Salaam, Septemba 23, 2026, ambapo pamoja na mambo mengine alieleza umuhimu wa ushirikiano wa karibu katika uendeshaji wa shughuli za Shirika majini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kiula amesema TAFICO iko katika hatua za mwisho za kumpata mbia kwa ajili ya kuanza shughuli za uvuvi na kusisitiza kuwa masuala ya usalama yanapewa kipaumbele katika uendeshaji wa meli za Shirika.
“Meli inapaswa kulindwa saa 24 kwa maslahi ya Taifa. Hivyo usalama wa meli hii na nyingine zitakazonunuliwa na Serikali ni jukumu letu sote, ndio maana leo nimekuja tujadiliane eneo hili muhimu la kuhakikisha tunakuwa na uendeshaji salama wa shughuli za Shirika,” alisema Dkt. Kiula.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Rear Admiral Ameir Ramadhani Hassan, amempongeza Dkt. Kiula kwa kuteuliwa kuiongoza TAFICO, akieleza kuwa jukumu hilo ni kubwa na linahitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali.
Rear Admiral Hassan amesema Jeshi la Wanamaji litaendelea kushirikiana na TAFICO katika maeneo ya pamoja, ikiwemo kukabiliana na uvuvi haramu na kutoa msaada wa kitaalam pale itakapohitajika.
Ushirikiano huo unalenga kuimarisha ulinzi wa shughuli za TAFICO zinazofanyika baharini, ikiwemo uendeshaji wa meli za uvuvi za Shirika katika Bahari Kuu, huku Jeshi la Wanamaji likiwa na nafasi muhimu katika kulinda usalama wa bahari ya Tanzania na kusaidia kukabiliana na vitendo vya uvuvi haramu na uhalifu mwingine unaofanyika majini.