TAFICO KATIKA MAPINDUZI SEKTA YA UVUVI, SERIKALI IKILENGA ASILIMIA 10 YA MCHANGO PATO LA TAIFA
Serikali imeeleza dhamira ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya uvuvi nchini kwa kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa, kutoka asilimia 2.2 ya sasa hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2050, kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu, kuimarisha uwezo wa uvuvi wa bahari kuu na kufufua shughuli za uvuvi wa kibiashara.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh, wakati akifungua hafla ya kuadhimisha mafanikio ya Programu ya Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe wa Majini kwa Mageuzi Endelevu Tanzania (FISH4ACP), iliyofanyika leo Oktoba 13, 2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Ili kufikia lengo kubwa la kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa kutoka asilimia 2.2 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2050, serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya uvuvi, ikiwemo ujenzi wa Bandari ya kipekee ya Uvuvi ya Kilwa, ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100, na kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), Shirika pekee la umma linalojihusisha na uvuvi wa kibiashara, ili kuongeza uwezo wa Serikali kushiriki moja kwa moja katika uzalishaji na matumizi ya rasilimali za uvuvi,” alisema Prof. Sheikh.
Prof. Sheikh ameongeza kuwa Serikali ina mpango wa kununua meli nne(4) za uvuvi ifikapo mwaka 2027 ili kuimarisha shughuli za uvuvi na kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi nchini, na kuanzisha Mamlaka ya Uvuvi Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi na maendeleo ya shughuli za uvuvi nchini.
FISH4ACP ni programu iliyoanzishwa na Shirika la Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS)ambapo Tanzania ni mwanachama, inayotekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) na Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani (BMZ).
Nchini Tanzania, programu hii ni ya miaka sita (2020–2026) na inalenga kuendeleza na kuimarisha mnyororo wa thamani wa uvuvi wa dagaa na samaki katika Ziwa Tanganyika.
Mwelekeo huu unaendana na jitihada za Shirika TAFICO za kuendeleza uvuvi wa kibiashara, kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi na kuchochea matumizi yenye tija ya rasilimali za maji nchini.