Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

"TAFICO NI MTOTO WETU"—KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE

Imewekwa: 07 August, 2026
"TAFICO NI MTOTO WETU"—KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imesema ina wajibu wa kuhakikisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) linaendelea kuimarika na kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb), leo Agosti 07,2026, wakati wa ziara ya Kamati kwenye banda la TAFICO, katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Kamati imetembelea TAFICO kwa lengo la kujionea maendeleo ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Shirika katika kuimarisha sekta ya uvuvi nchini. Akiwa katika banda la TAFICO, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, pamoja na wajumbe wa Kamati, walipokea maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati na hatua zilizofikiwa, yaliyowasilishwa na Afisa Uvuvi Mwandamizi wa TAFICO, Bw. Mgalula Lyobah.

Baada ya kupokea maelezo hayo, Mhe. Mwanyika alieleza kuridhishwa na hatua zinazopigwa na Shirika katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuendeleza sekta ya uvuvi wa kisasa na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

"TAFICO ni mtoto wetu. Ni wajibu wetu kuhakikisha linaendelea kuimarika na kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali. Tunafurahishwa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ambayo itaongeza tija, ajira na mchango wa sekta ya uvuvi katika maendeleo ya nchi," alisema Mhe. Mwanyika.

Kwa upande wake, Bw. Lyobah alieleza kuwa TAFICO inaendelea kutekeleza kwa ufanisi miradi ya kimkakati inayolenga kukuza uvuvi wa bahari kuu, ikiwemo ununuzi wa meli 4 ambazo ziko katika hatua ya ununuzi na kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu wezeshi . Kukamilika kwa miundumbinu hii kuna kwenda sambamba na kukamilika kwa ujenzi wa bandari ya uvuvi iliyojengwa na Serikali Kilwa Masoko hizi ni jitahada za Serikali katika kuleta mapinduzi katika sekta ya uvuvi nchini.

"Hatua hizi zinakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya kuendeleza uchumi wa buluu na kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinatumika kwa manufaa ya watanzania," alisema Bw.Mgalula.

TAFICO inaendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli zake, huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu.