Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

MWENYEKITI BODI YA WAKURUGENZI TAFICO ASISITIZA MAADILI NA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI

Imewekwa: 20 September, 2026
MWENYEKITI BODI YA WAKURUGENZI TAFICO ASISITIZA MAADILI NA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), Prof. Yunus Daud Mgaya, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa watumishi wa Shirika, akieleza kuwa maadili ni msingi muhimu wa kulifikisha Shirika katika malengo yake ya kuwahudumia wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Prof. Mgaya ameyasema hayo Septemba 18, 2026, wakati akizungumza na Watumishi wa TAFICO katika Ofisi za Makao Makuu Kigamboni Dar es Salaam, katika kikao kilicholenga kuongeza uelewa kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma kwa Watumishi wa Umma.

Katika mazungumzo hayo, Prof. Mgaya amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kuzingatia misingi ya maadili katika utekelezaji wa majukumu yao, akitaja mambo matatu muhimu ambayo yanapaswa kupewa uzito katika utendaji wa kila siku; kuwa na utaalamu katika kazi, Uaminifu na Uwajibikaji.

"Kwa TAFICO kufikia malengo yake ya kutoa huduma kwa wananchi na kutekeleza majukumu yake katika maendeleo ya sekta ya uvuvi, maadili ya utumishi wa umma yanapaswa kuwa sehemu ya msingi ya utendaji wa kila mtumishi", aliongeza Prof. Mgaya.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, Dkt. Suleiman Kiula, ndc, amemshukuru Mwenyekiti wa Bodi kwa kutenga muda wa kuzungumza na watumishi kuhusu suala hilo muhimu, akieleza kuwa ujumbe huo ni sehemu muhimu ya kuendelea kujenga uelewa na utamaduni wa uwajibikaji ndani ya Shirika.

Kikao hicho ni mwendelezo wa utaratibu ambao shirika umejiwekea wa kukutana kila Ijumaa kuzumza masuala mbalimbali ya kiutendaji kwa dhamira mbalimbali ikiwemo kujenga desturi ya watumishi kufahamu mambo yanayoendelea na kuhamassha mshikamano na ushirikiano.