Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

WADAU WAKUTANA KUPANGA KUIFANYA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO KUWA CHACHU YA UCHUMI

Imewekwa: 12 September, 2026
WADAU WAKUTANA KUPANGA KUIFANYA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO KUWA CHACHU YA UCHUMI

Wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi na huduma zinazohusiana na bandari wamekutana leo Septemba 12, 2026 katika Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko, Mkoa wa Lindi, kujadili maandalizi ya uendeshaji wa bandari hiyo na kuweka mazingira yatakayowezesha kuanza kwa shughuli zake kwa ufanisi.

Kikao hicho kimeandaliwa na Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na kuwakutanisha wawakilishi kutoka Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, TANESCO, Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe (BMU) na Mamlaka ya Maji Kilwa, na kujadiliana namna ya kuhakikisha kila taasisi inatekeleza kwa ufanisi majukumu yake ili bandari hiyo iweze kutoa huduma kikamilifu.

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Mohamed Nyundo, amesema Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko ni chachu ya kuboresha maisha ya Watanzania na kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana katika eneo moja, ili kurahisisha na kuharakisha taratibu za upakuaji na utoaji wa samaki, kuondoa urasimu na kuepusha ucheleweshaji unaoweza kuathiri shughuli za uvuvi na biashara ya mazao ya baharini.

Amesema wadau hao wamekutana kwa lengo la kuhakikisha bandari hiyo inaanza kufanya kazi kwa ubora unaostahili, huku ikiweka mazingira rafiki ya kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara kushiriki katika shughuli mbalimbali zitakazochochewa na uwepo wa bandari hiyo. “Wadau mmekutana ili tuanze kwa ubora na kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara. Kila taasisi inatakiwa kutoa huduma zake zote hapa hapa bandarini ni lazima tuwe na kituo cha huduma zote muhimu (one stop centre),” amesema Mhe. Nyundo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO Dkt. Suleiman Kiula, ndc , amesema miundombinu yote muhimu kwa ajili ya kuanza kwa shughuli za uendeshaji wa bandari hiyo ipo tayari. “Kwa upande wetu, kila kitu kiko tayari kuelekea uzinduzi wa bandari. Miundombinu ipo, wataalamu wapo na tunaendelea kuimarisha uwezo wao kupitia mafunzo. Pia tuna meli ambayo muda wowote itakuja kuegeshwa hapa bandarini,” amesema Dkt. Kiula.

Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko inatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha shughuli za kiuchumi katika sekta ya uvuvi, kwa kuongeza fursa za uwekezaji, biashara, ajira na huduma zinazohusiana na mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi, sambamba na kuongeza mapato ya Serikali.