WATUMISHI TAFICO WAASWA KUWA WABUNIFU

MKURUGENZI wa Ufuatiliaji na Tathmini Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bwana. Daudi Mayeji amewataka watumishi wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kuwa wabunifu katika utoaji wa maoni na mawazo juu ya uendelezwaji wa Shirika, ili kufikia malengo ya taasisi hiyo.
Bw. Mayeji amesema hayo leo Aprili 8, 2025 wakati akizindua baraza la wafanyakazi katika ofisi za TAFICO, zilizopo eneo la Ras Mkwavi Kigamboni, Dar es salaam.
Bw. Mayeji ambaye katika hafla hiyo alimuwakilisha Naibu Waziri Wizara ya Mfugo Uvuvi, amesema baraza la wafanyakazi ni kiungo muhimu katika kufikia malengo ya shirika ikiwa watumishi watashirikishwa kikamilifu katika kubuni miradi yenye tija.
“Nitoe wito kwa watumishi kutoa maoni na mawazo ya kibunifu yanayolenga kukuza shirika ili lifikie malengo yake ya kufanya shughuli za uvuvi katika bahari kuu na hivyo kuliingizia kipato kwa maslahi mapana ya Taifa letu,” amesema Bw. Mayeji.
Vilevile, alieleza juu ya nia ya Serikali kupitia wizara kuendelea kiliimarisha shirika kwa kuhakikisha linapata watumishi wenye utaalam na ujuzi wa biashara, uendeshaji wa meli za uvuvi na fedha kwa ajili ya uwekezaji.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya taasisi kwa niaba Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika, Meneja wa Huduma za Shirika, Bw. Ahmed Byabato amesema uundwaji wa baraza hilo la wafanyakazi ni utekelezaji wa dhana nzima ya utawala bora.
Bw. Byabato amesema baraza hilo linalilozinduliwa leo, litaanza kazi mara moja ambayo ni kupitia na kupitisha bajeti ya mwaka 2025/26 ya Shirika, ambapo makadirio ya bajeti hiyo ni Shilingi bilioni 5.48.
“Ushirikishwaji wa watumishi kupitia baraza kutawezesha umiliki wa pamoja wa shughuli zinazotekelezwa na shirika hivyo kuleta matokeo chanya katika utekelezaji wa mipango iliyopo”. amesema Bw. Byabato.
Baraza la wafanyakazi ni chombo kinachoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini namba 6 ya mwaka 2004 na Tamko la Serikali namba 1 la mwaka 1970 juu ya ushirikishwaji wa watumish katika masuala mbalimbali ya taasisi.