Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

KATIBU MKUU WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI AZINDUA MTAMBO WA KUZALISHA BARAFU TAFICO

Imewekwa: 13 March, 2025
KATIBU MKUU WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI AZINDUA MTAMBO WA KUZALISHA BARAFU TAFICO

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amezindua mtambo wa kuzalisha barafu za tofali (block ice) wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), kwenye hafla ya makabidhiano na uzinduzi iliyofanyika tarehe 07 Machi 2025, Makao Makuu ya Shirika hilo, Ras Mkwavi, Kigamboni Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Prof. Shemdoe amesema mtambo huo wenye uwezo wa kuzalisha tani 5 kwa siku uliokabidhiwa na Kampuni ya Albacore ya Afrika Kusini utasaidia kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi kwa kuongeza upatikanaji wa barafu kwa matumizi ya Shirika, wavuvi na wauzaji wa samaki kwenye soko la Feri, Kilwa, Lindi na maeneo mengine.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu TAFICO CPA Shaibu Matessa amesema ujio wa mtambo huo ni muhimu kwani utawezesha kuendeleza utekelezaji wa miradi tisa (9) iliyopo kwenye Mpango wa Biashara wa TAFICO wa miaka kumi (2023-2033), Kati ya miradi hiyo ni uzalishaji wa barafu kwa ajili ya kusaidia kupunguza upotevu wa mazao ya Uvuvi baada ya kuvuliwa, hivyo kuongeza tija kwa Shirika na wavuvi wengine.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa
Bahari Kuu (DSFA) Dkt. Emmanuel Sweke, Muwakilishi wa kampuni ya Albacore, Bw. Andrew Thompson, wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali, na wadau wengine wa uvuvi.