Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

DKT. KIULA AWASILI RASMI TAFICO, AHIMIZA UWAJIBIKAJI NA UBUNIFU

Imewekwa: 26 August, 2026
DKT. KIULA AWASILI RASMI TAFICO, AHIMIZA UWAJIBIKAJI NA UBUNIFU

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), Dkt. Suleiman Peter Kiula, ndc, Agosti 14, 2026, amewasili rasmi ofisi za Makao Makuu ya Shirika zilizopo Kigamboni Dar es Salaam, na kuzungumza na watumishi wa Shirika, akisisitiza umuhimu wa mshikamano, nidhamu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu ya TAFICO.

Dkt. Kiula amesema TAFICO ina majukumu makubwa katika mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi, ikiwemo uendeshaji wa meli, bandari, viwanda vya uchakataji wa mazao ya uvuvi pamoja na kuingia katika ufugaji wa samaki.

Katika kuyafanikisha malengo ya Shirika, Dkt. Kiula ametoa rai kwa watumishi kuwa sehemu ya Shirika na kila mmoja kuwa kiongozi katika eneo lake la utendaji, huku akisisitiza nidhamu na ushirikiano.

“Tutasimama pamoja, tutashirikiana ili tutengeneze historia ya sekta ya uvuvi nchini. TAFICO inaanza safari ya kwenda kuingia bahari kuu,” alisisitiza.