Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

UJUMBE WA MFUKO WA KIMATAIFA WA MAENDELEO YA KILIMO WATEMBELEA TAFICO

Imewekwa: 09 November, 2024
UJUMBE WA MFUKO WA KIMATAIFA WA MAENDELEO YA KILIMO WATEMBELEA TAFICO

Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), ambao unafadhili Programu ya Maendeleo ya Kilimo na Uvuvi (AFDP) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, pamoja na watekelezaji wa programu hiyo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, umetembelea Makao Makuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) Ras Mkwavi Kigamboni kuzungumzia miradi iliyopo kwenye Programu hiyo 08 Novemba 2024.

Kikao hicho kiliongozwa na Kaimu Mtendaji Mkuu TAFICO CPA Shaibu Matessa na kuwahusisha wadau wengine wa maendeleo na mazingira, ambapo Mratibu wa Mradi kwa upande wa TAFICO Bw. Mgalula Lyoba alitoa wasilisho kuhusu hali ya utekelezaji wa miradi ya programu.

Kupitia pragramu hiyo TAFICO itanufaika na miradi mikubwa mitano ambayo ni Ununuzi wa meli nne za uvuvi wa Bahari Kuu za TAFICO, ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki kinachotarajiwa kujengwa wilayani Kilwa, ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chakula cha samaki kinachotarajiwa kujengwa kati ya Mwanza na Dodoma, mtambo wa kuzalisha barafu na magari mawili ya ubaridi.

Walioshiriki ni pamoja na Mratibu wa Mradi kwa upande wa AFDP Bw. Salim Mwinjaka, Bw. Richard Abila kutoka IFAD, wawakilishi kutoka TAMISEMI, PCU, watekelezaji wengine wa programu na menejimenti ya TAFICO.