Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

BUNGE LAKOSHWA NA UWEPO WA MELI YA KWANZA YA UVUVI NCHINI

Imewekwa: 13 March, 2026
BUNGE LAKOSHWA NA UWEPO WA MELI YA KWANZA YA UVUVI NCHINI

◼️Nyingine 2 zipo kwenye mchakato wa manunuzi

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzani kupitia Kamati yake ya kudumu ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imefurahishwa na uwepo wa meli ya kwanza ya Uvuvi nchini iliyotia nanga kwenye gati la Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) siku chache zilizopita.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika mara baada ya kukagua utendaji kazi wa meli hiyo wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyofanywa kwenye shirika hilo Machi 13,2026 jijini Dar-es-salaam.

“Tumefarijika sana kama kamati kwa sababu jambo hili la meli ni jambo lililoongelewa ndani ya bunge kwa muda mrefu sana tangu 2021 na kwenye usimamizi wetu moja ya mambo tuliyoyaona ni kuona mchango wa sekta ya Uvuvi unaweza kuwa mkubwa zaidi ya hapa ulipofika” Ameongeza Mhe. Mwanyika. Aidha Mhe. Mwanyika amesisitiza kuwa sekta hiyo inagusa watu wa kawaida hivyo endapo watapatikana samaki wa kutosha wanaweza kuuzwa ndani ya mkoa wa Dar-es-salaam na nje ya hapo na hivyo kunufaisha kundi la watu wengi waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya Uvuvi.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza jambo hilo la kihistoria ambapo ameahidi kuhakikisha sekta hiyo inaongeza mchango wake kwenye pato la Taifa ndani ya miaka 5 kutoka asilimia 1.7 hadi asilimia 10 ifikapo 2030.

Naye Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Mhe. Hadija Aboud amebainisha kuwa uwepo wa meli hiyo umeakisi usikivu wa Serikali kwenye masuala yanayogusa wananchi moja kwa moja ambapo ameaishauri kuendelea kuwekeza fedha zaidi kwenye Shirika hilo ili likamilishe kazi zote na kuanza kazi. “Tukiendelea kuwekeza kidogo kidogo itasababisha miundombinu iliyotengenezwa awali kuchakaa kabla haijatumika na hapa kuna fedha nyingi sana hata wananchi na wavuvi wanajua hilo” Amehitimisha Mhe. Aboud.