JUHUDI ZA PAMOJA ZINAHITAJIKA KULINDA BAHARI- DKT. MPANGO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema zinahitajika juhudi za pamoja za ndani ya nchi, kikanda na kimataifa katika kuweka mikakati ya kulinda rasilimali za bahari vinginevyo ifikapo mwaka 2050 bahari itakuwa imeelemewa.
Makamu wa Rais alisema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam leo tarehe 08 Juni 2023.
Alisema inapaswa kuwepo kwa uwiano sawia kati ya hali ya bahari na kuimarika kwa uchumi kwani Afya ya Bahari na mifumo imara ya kiikolojia ya baharini ni muhimu kwa uchumi wa buluu ambao ni sehemu ya ajenda ya nchi kufikia maendeleo endelevu.
Dkt. Mpango aliongeza kwamba tafiti zinaonesha kufikia 2030 Bahari itakuwa ndio nguzo kuu ya uchumi duniani ambapo takriban watu milioni 40 watakuwa wameajiriwa moja kwa moja na viwanda vinavyotumia rasilimali za bahari.
Aidha, Makamu wa Rais aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi za Utafiti wa Bahari kama Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Taasisi ya Sayansi za Bahari iliyoko Zanzibar (IMS) kuhakikisha utafiti wa kina unafanyika kwa wingi zaidi ili kuongeza uelewa wa sayansi ya bahari pamoja na athari za changamoto zilizojitokeza kwa jamii na ikolojia.
Vilevile Makamu wa Rais amesema upo umuhimu mkubwa wa kuhusisha na kushirikishwa kikamilifu kwa jamii za asili ya pwani katika ulinzi wa rasilimali za bahari kwa kuwa wao ndio wafaidika au waathirika wa kwanza wa mazingira ya bahari. Pia ameagiza Mamlaka zinazohusika na uvuvi na uhifadhi ziongeze jitihada katika kutoa elimu zaidi kwa wavuvi ili washiriki kikamilifu katika uhifadhi wa rasilimali endelevu za bahari na kuondokana na njia zisizofaa za uvuvi.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema Wizara hiyo inatoa umuhimu mkubwa katika shughuli za uhifadhi wa rasilimali za bahari na kudhamiria kuilinda bahari na viumbe wake. Ameongeza kwamba ili kuwa na uvuvi endelevu ni lazima kuwa na maeneo ya uhifadhi baharini ambayo yanalenga katika kulinda, kuhifadhi na kudumisha uvuvi endelevu na kukuza mchango wa sekta ya uvuvi na pato la taifa.
Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde alisema kuwa pamoja na changamoto ya matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imekuwa moja ya kisababishi cha uharibifu wa mazingira ya bahari, yeye pamoja na Waziri Ulega wamedhamiria kuhakikisha kuwa wanaendelea kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za Bahari ili ziendelee kuchangia vyema kwenye uchumi wa buluu.
Kauli Mbiu ya Siku ya Bahari Duniani kwa mwaka 2023 ni “Sayari ya Bahari: Mawimbi Yanabadilika” (Planet Ocean: Tides Are Changing)