Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

SERIKALI KUIMARISHA UVUVI WA BAHARI KUU KUPITIA SHIRIKA LA UVUVI TANZANIA (TAFICO)

Imewekwa: 14 May, 2026
SERIKALI KUIMARISHA UVUVI WA BAHARI KUU KUPITIA SHIRIKA LA UVUVI TANZANIA  (TAFICO)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema Serikali inaendelea kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kwa kulipatiavitendea kazi vya kisasa na kuendeleza miundombinu ya uvuvi ili kuongeza tija katika sekta hiyo na kukuza uchumi wa buluu nchini.


Akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo Bungeni mjini Dodoma leo Mei 14, 2026, kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Dkt. Bashiru alisema Serikali, kupitia ufadhili wa Programu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii ya Japan, imepokea meli ya kisasa ya uvuvi wa bahari kuu, TAFICO FV.01. Meli hiyo ilizinduliwa rasmi Aprili 25, 2026 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Alisema ujio wa meli hiyo ni hatua muhimu ya kuongeza uwezo wa Tanzania kuvuna rasilimali za uvuvi katika Ukanda Maalum wa Uchumi wa Bahari (EEZ), pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa na ajira.


Waziri huyo aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imekamilisha ukarabati wa gati maalum la kushusha na kupandishia mazao ya uvuvi katika meli (floating jetty) lililopo Ras Mkwavi, ambalo sasa liko tayari kuhudumia shughuli za meli za uvuvi wa bahari kuu na kuongeza ufanisi wa shughuli za Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).


Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imepanga kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta ya uvuvi, ikiwemo: Kukamilisha ununuzi wa meli mbili za uvuvi wa bahari kuu; Kukamilisha usanifu wa kina na kuanza ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Bagamoyo; Kuendelea Kuimarisha ulinzi wa rasilimali za uvuvi; Kutafuta na kupanua masoko ya bidhaa za uvuvi ndani na nje ya nchi; Ujenzi wa miundombinu ya kuimarisha mnyororo wa thamani kwa mazao ya uvuvi.


Katika hatua nyingine, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), ikiwemo ukarabati wa ghala la kuhifadhi samaki kwa ubaridi, kiwanda cha uchakataji wa mazao ya uvuvi pamoja na uzalishaji wa chakula cha samaki. Serikali pia inaendelea kuongeza vifaa vya kisasa vya uchakataji na uhifadhi wa samaki ili kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.


Aidha, Serikali inalenga kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya uvuvi wa kisasa, hatua inayokusudiwa kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na rasilimali za Bahari Kuu. Ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, ambayo inalenga kuongeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kwa asilimia 70.