Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

TAFICO YAJIPANGA KUPOKEA MELI YAKE YA KWANZA YA KISASA YA UVUVI

Imewekwa: 28 January, 2026
TAFICO YAJIPANGA KUPOKEA MELI YAKE YA KWANZA YA KISASA YA UVUVI

Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, CPA Shaibu Matessa amefanya kikao cha maandalizi ya mapokezi ya meli ya kwanza ya kisasa ya uvuvi ya Shirika, ikiwa ni sehemu ya hatua za kimkakati kuelekea kuanza rasmi kwa shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu nchini. Kikao hicho kimefanyika tarehe 23 Januari 2026.

Kikao hicho kimewakutanisha wataalam wa taasisi zote muhimu za Serikali zinazohusika moja kwa moja katika mchakato wa mapokezi ya meli hiyo, zikiwemo Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Aidha, mkandarasi wa ujenzi wa meli hiyo aliyeko nchini Vietinam ameshiriki kwa njia ya mtandao.

Majadiliano ya kikao yamejikita katika masuala muhimu yanayohusu safari ya meli kutoka nchini Vietinam hadi Tanzania, ikiwemo ratiba na muda wa safari, utaratibu wa usafirishaji wa chombo katika maji, maandalizi ya upokeaji katika Bandari ya Dar es Salaam na kufikishwa meli hiyo katika gati la TAFICO Ras Mkwavi, Kigamboni.

Maeneo mengine ni kujadili taratibu za kisheria, kiusalama na vibali vinavyohitajika meli itakapowasili nchini. Msisitizo mkubwa umewekwa kwenye umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi husika ili kuhakikisha mchakato wa mapokezi unafanyika kwa ufanisi, kwa wakati, na kwa kuzingatia sheria na kanuni za usafiri wa vyombo vya baharini.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa TAFICO, CPA Shaibu Matessa, amesema kuwa maandalizi ya mapokezi ya meli hiyo yana umuhimu wa kimkakati kwa nchi na kwa sekta ya uvuvi kwa ujumla.

Ameeleza kuwa ujio wa meli hiyo ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza ajenda ya Uchumi wa Buluu na Dira ya Taifa 2050 inayolenga maendeleo ya viwanda, kuongeza upatikanaji wa mazao ya uvuvi kwa soko la ndani, kufungua masoko ya kimataifa, pamoja na kuchochea uongezaji thamani wa mazao ya uvuvi.

Meli hiyo imejengwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Kiuchumi na ya Kijamii (ESDP) ya Serikali ya Japan, na kwa sasa maandalizi ya mwisho ya usafirishaji yanaendelea.