Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

TAFICO YAPOKEA UJUMBE WA WATAALAMU WA UCHUMI WA BULUU KUTOKA SOMALIA KUBADILISHANA UZOEFU

Imewekwa: 17 July, 2026
TAFICO YAPOKEA UJUMBE WA WATAALAMU WA UCHUMI WA BULUU KUTOKA SOMALIA KUBADILISHANA UZOEFU

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) limepokea ujumbe wa wataalamu wa Uchumi wa Buluu kutoka Serikali ya Shirikisho la Somalia waliotembelea shirika hilo kujifunza namna Tanzania inavyotekeleza shughuli za uvuvi wa bahari kuu na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.

Katika ziara iliyofanyika Julai 15, 2026, ujumbe huo ulitembelea miundombinu mbalimbali ya TAFICO ikiwemo mtambo wa kuzalisha barafu, ghala la ubaridi, magari ya ubaridi ya kusafirisha mazao ya uvuvi pamoja na meli ya uvuvi wa bahari kuu ya TAFICO FV.01, ambapo ulipata maelezo kuhusu mchango wa uwekezaji huo katika kukuza uchumi wa buluu na usalama wa chakula.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ndg. Christian Nzowa, alisema ujumbe huo upo nchini kwa ziara ya mafunzo ya siku mbili yenye lengo la kujifunza uzoefu wa Tanzania katika uratibu wa shughuli za Uchumi wa Buluu, usimamizi wa uvuvi, uhifadhi wa rasilimali za baharini, mifumo ya kisheria pamoja na uongezaji wa thamani wa mazao ya bahari.

Kwa upande wake, Meneja wa Mipango na Ubia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa TAFICO, Bw. Baraka Maduhu, ndc, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, alisema Shirika linaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na uvuvi wa bahari kuu ili kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao ya uvuvi na fursa za ajira.

Bw. Maduhu alieleza kuwa TAFICO itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kubadilishana uzoefu na teknolojia zitakazochochea maendeleo ya Uchumi wa Buluu na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa taifa.