Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA RASMI UJENZI WA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO, MKOANI LINDI

Imewekwa: 19 September, 2023
RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA RASMI UJENZI WA BANDARI YA UVUVI KILWA MASOKO, MKOANI LINDI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Septemba 19, 2023 amezindua rasmi uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa katika tukio lililofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi.

Kukamilika kwa bandari hiyo kutawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Pia, uwepo wa bandari ya uvuvi utachochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi. Hivyo, uwekezaji huu, unaenda kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kutoka tani 40,721.53 zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 249.54 hadi tani 52,937.99 na kuchangia takriban asilimia 10 katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2036.

Aidha, Bandari hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira kwa watanzania takriban 30,000 huku katika hatua za awali za ujenzi, jumla ya ajira za muda mfupi 278 zimetolewa ambapo kati ya hizo ajira 106 sawa na asilimia 38 zimetolewa kwa wakazi wa wilaya za Mkoa wa Lindi.