KATIBU MKUU WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI ARIDHISHWA NA UKAMILIKAJI WA GATI LA TAFICO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, Februari 15, 2026 amepokea mradi wa ukarabati wa gati la kuegeshea meli (floating jetty) wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), uliopo Makao Makuu ya Shirika Ras Mkwavi, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Akipokea mradi huo, Katibu Mkuu ameridhishwa na kukamilika kwa ukarabati wa gati hilo ambalo limekamilika kwa zaidi ya 98%, huku kazi zilizobaki zinatarajiwa kukamilika tarehe 18 Februari 2026.
Ukarabati wa gati hili ni maandalizi ya upokeaji wa meli ya Uvuvi wa bahari kuu ambayo itaendeshwa kwa ubia kati ya sekta binafsi na Serikali .
Akipokea taarifa ya maandalizi ya mapokezi ya meli ambayo ilihusisha ukarabati wa gati na upatikanaji wa mbia , Bi. Meena amepongeza kwa hatua iliyofikiwa ya kumpata mbia wa uendeshaji wa meli.
Aidha, amewahimiza watumishi wa Shirika hilo kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu ili kuliinua shirika na kulifanya kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya uvuvi nchini.
TAFICO inatarajia kupokea meli ya Uvuvi wa Bahari Kuu , meli hiyo na miradi inayotekelezwa inalenga kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, kuimarisha ajira pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa buluu nchini.